Barua ya wazi kwa Rais Jakaya Kikwete

November 6, 2006 at 11:37 pm 2 comments

*Kama nilivyoipokea toka kwa R.L, rafiki yangu wa miaka mingi toka TZ.

Ndugu Yesse,

Salamu!

Mimi mzima namshukuru Mungu sana.

Asante kwa maombi yako kwani Jumamosi ilikuwa nzuri sana na yenye mafanikio lukuki.

Huku Bongo namba za simu zimebadilika ndo maana umepata shida kunipata.

Nimepata hii maneno ya mmoja kati kundi kuuuubwaaaaa la Wabongo wanavyofikiria kuhusu EAC na mchakato wa kuanzisha jumuia; najua utapata point kwenye shughuli zako.

NISIKUPOTEZEE MUDA SANA NAJUA SIKU HIZI UKO BUSY THAN EVER.

******

BURIANI TANZANIA … AU KILA LA HERI AFRIKA MASHARIKI?
Na Mlenge Fanuel
“Mtu akikushauri jambo la kijinga, huku anajua jambo hilo analokushauri ni la kijinga, na wewe ukakubali, basi atakuona, wewe zuzu!” — Mwalimu Julius K. Nyerere,  1994/5
Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tafadhali isome barua hii ya wazi ya kukufikishia ujumbe kwamba Tanzania haiko
tayari kujiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki (East African Federation, EAF) wala “Soko la Pamoja” la Afrika Mashariki, na kwamba Watanzania hatutaki Tanzania ijiunge na Shirikisho hilo.

Yatakuwa ni maafa makubwa kwa Tanzania na Watanzania iwapo Tanzania itajiunga na EAF hasa kwa mpangilio ulioko wa ” fast track”. Ndiyo maana nimeanza na nukuu ya Mwalimu Nyerere, ambaye tayari baadhi ya watu, hasa wa nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda, wameanza kumsingizia kwamba kwa kujiunga na EAF tutakuwa
“tunamuenzi” Mwalimu Nyerere, huku wakijua fika ushauri wanaotupa wa kujiunga na Shirikisho na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki hauna manufaa yoyote kwa
Tanzania, wakidhania sisi Watanzania ni mazuzu tunaoendekeza wema wa mshumaa kuwaangazia wengine huku wenyewe unateketea, kwa minajil ya kupata misifa isiyo
na tija.
Ni kweli Mheshimiwa Rais umeunda Tume ya Kupokea Maoni kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini inatia mashaka iwapo huo siyo tu ni utaratibu uliouweka
kuhalalisha maamuzi yaliyokwishafikiwa ya kuidumbukiza Tanzania kwenye EAF.

Hii inatokana na muonekano kwamba Tanzania kujiunga na EAF kumeshaamuliwa tayari — kutaka watu tujadili siyo kiinimacho tu?

Mheshimiwa Rais, palikuwa na muswada uliopelekwa Bungeni wa Tanzania kujiunga na EAF, ambao Waheshimiwa Wabunge waliukataa, na serikali ikabidi iuondoe. Lakini
mchakato wa Tanzania kujiunga na EAF ukaendelea tu, na kupuuza maoni ya Wabunge wetu tuliowachagua watuwakilishe.

Ikiwa sikusikiliza vibaya, katika Bunge la Bajeti 2006/2007, Mheshimiwa Waziri wa Afrika Mashariki aliliambia Bunge kwamba patakuwa na KURA YA MAONI kuhusu Afrika Mashariki.

Matokeo yake tumeletewa Tume badala ya kura ya maoni! Kana kwamba hiyo
haitoshi, iliripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa wewe Mheshimiwa Rais wetu, ulimhakikishia Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwamba utafanya kila unaloweza
kuhakikisha kufanikiwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, kwenye mkutano wenu uliofanyika Mwanza.

Je, maoni tunayotoa Watanzania kukataa kujiunga na shirikisho si “kilio cha samaki — machozi yanakwenda na maji?” Wenyewe “wenye nchi” mshaamua mloamua?  Pana maswali mengi mheshimiwa Rais ambayo ukitupatia majibu utakuwa umetuwezesha Watanzania tulio wengi kuelewa kuhusu mustakabala wa maisha yetu na Tanzania
yetu:
* Je, Ni sera ya CCM Tanzania kujiunga na EAF au Soko la Pamoja la Afrika Mashariki?
* Je, Ilikuwa kwenye ilani ya Uchaguzi 2005 ya Chama Tawala CCM Tanzania kujiunga na EAF?
* Je, Nani aliyependekeza Tanzania ijiunge na EAF? (Inabidi tumfahamu ili tuweze kumpamba maua iwapo Tanzania itafanya tunalodhani ni kosa la maisha la
kujiunga EAF kumbe ikathibitika EAF ni manufaa tele kwa Tanzania ; vinginevyo inabidi tumfahamu ili tuweze kumzomea na kumuimbia nyimbo za kumsimanga pindi
machungu ya EAF yatakapoanza kudhihirika muda si muda iwapo Tanzania itafanya kosa la maisha kujitumbukiza kwenye EAF. Vinginevyo itakuwa kama mikataba ya madini — hatuelezwi nani aliwaalika na kuingia mikataba na ‘wawekezaji’ kwenye migodi.)
* Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameshajitangaza kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki — ikiwa na maana yote mengine yanayojitokeza sasa ni
kuhalalisha na kusafisha njia ya Museveni kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki, hasa ukitilia maanani Rais wa Kenya na wewe Rais wetu mko
kimya, ikielekea mmekubaliana na matamshi ya Museveni. Si hivyo?
* Kutokana na maneno yanayosemwa na Wakenya na Waganda, Wanyarwanda na Warundi, inaonekana kama vile serikali ya Tanzania HAINA UBAVU wa kusema HAPANA kwa EAF — kila mara Tanzania inazomewa inapohoji maslahi yake kwenye EAF — au inapotaka kutumia uhuru wake ISIJIUNGE na EAF. Hivi karibuni Waziri wa Afrika Mashariki wa Tanzania alisemwa kwenye vyombo vya habari kwamba hahudhurii vikao vya Afrika Mashariki — na kumfanya Mheshimiwa Waziri Mkuu ajitokeze kumtetea — na baadaye Waziri yule akaondoshwa toka Wizara ya
Afrika Mashariki kwenye mabadiliko ya Baraza la Mawaziri uliyoyafanya hivi karibuni Mheshimiwa Rais.
Ina maana Tanzania ni kama mbwa anayeelekea kwenye mdomo wa chatu EAF — amefyata mkia, anatoa kilio cha mwisho, na hana la kufanya zaidi ya kufanywa asusa na kumezwa — au si hivyo?
* Ni kwa nini Kiswahili SIYO lugha rasmi EAC, na badala yake ni kiingereza?
* Kama shida ni ushirikiano, kwa nini Tanzania isijiunge na Msumbiji na Zambia , na kutengeneza shirikisho?
* Kwa nini EAF inaharakishwa namna hii?
* Ni nini Tanzania inahitaji kwenye EAF ambacho haiwezi kukipata bila kuwemo kwenye shirikisho hilo ? (Mbali na ngonjera za kisiasa, pengine na watu fulani kupata posho za vikao vya EAC na baadhi kuandikwa kwenye vitabu vya historia, vitu ambavyo havimsaidii Mtanzania mpiga kura wako anayesubiri neema tele na
maisha bora…)
* Pana bidhaa zipi za Tanzania hazifiki kwenye soko Kenya au Uganda , ambazo EAF itazifanya zifike sokoni?
* Nani atakuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Afrika Mashariki, na ni upi mchango wa EAF kwenye uvamizi dhidi ya DRC?
* Mheshimiwa Rais, hivi “Usalama wa Taifa” wa Tanzania una majukumu gani makubwa zaidi ya kulinda (uhuru) “Sovereignty” ya nchi yetu? Kwa nini “Usalama wa
Taifa” haukupi picha kamili ambayo itakufanya usijisumbue hata kuja kutuuliza iwapo tunataka uhuru wa nchi yetu uondoke kupitia “soko la pamoja” na “Shirikisho la Afrika Mashariki”, badala yake tukaendelea kulijenga taifa “letu changa” na kuulizana
maswala ya maendeleo kama vile tutanufaikaje na maliasili tulizojaaliwa nchini mwetu?
* Kwa kuitumbukiza Tanzania kwenye “Soko la Pamoja” la Afrika Mashariki, huoni kwamba utakuwa umekiuka kiapo ulichokula cha kuulinda uhuru wa, na mipaka ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ?
* Kulikuwa na sababu gani ya kupambana na Idd Amin aliyetaka kipande “kidogo tu” cha nchi yetu, ikiwa leo tunaigawa sandakarawe nchi nzima kwa kisingizio cha soko la pamoja?
* Tanzania itaondoka SADC? (Tayari nchi nyingine za Afrika Mashariki zimeanza kutuamuru tutoke SADC. SADC imeweka bayana kwamba wakati umefika wa kuchagua kati ya EAF au SADC.) Unadhani itakuwa ni busara kuondoka SADC? Kwa nini usitoe tamko kwamba Tanzania ya kesho ni ndani ya SADC?
* Je sisi wananchi wa Watanzania tutaulizwa kuhusu kujiunga na “Soko la Pamoja la Afrika Mashariki” au ni uamuzi uliofikiwa tayari kwamba tutajiunga na soko la pamoja la Afrika Mashariki?
* Huo Mkataba wa EAC/EAF uko wapi ili tuweze kuuona na kuusoma? Ni Watanzania gani waliousoma na kuuridhia kwamba SASA tunaanza kuwa kwenye mchakato wa kuelekea kwenye Shirikisho? (Inaripotiwa kwamba Tume yako ni sehemu tu ya taratibu ‘chovu’ za mchakato huo…)
Watanzania tutafanyaje ili kuondoka kwenye EAF, iwapo Tanzania ijajikaanga yenyewe kwa kuingia kwenye EAF?
Vipengele vya kujiondoa kwenye EAF viko wapi?
Hautakuwa ni uhaini kuzungumzia kujitoa EAF, kama ambavyo si ruksa kuzungumza kujitoa kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ?
Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, maswali hayo na mengine mengi yanaleta  changamoto kwako binafsi kwamba zawadi kubwa kuliko zote unazoweza kutupa sisi
Watanzania, ni kutukabidhi Tanzania yetu yenye “sovereignty” ileile au zaidi ya uliyokabidhiwa pale utakapoacha madaraka mwaka 2010 au 2015, panapo majaaliwa.
Kwa taarifa yako Mheshimiwa Rais , Tanzania ndiye “Mbuzi wa Shughuli” kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Na mbuzi huyu amepangwa “kuchinjiwa kwenye
maji” ili hata ukelele wake wa mwisho usisike.
Hawatarudia makosa ya Jumuia ile iliyokufa 1977, kwa kutuacha bado tunafurukututa. Kujiunga kwa Tanzania EAF kwafanana na Punda wa kwenye hadithi moja iliyochapishwa Tanzania ambamo Simba baada ya kujeruhiwa, alishindwa kuwinda; na Sungura, Fisi na Punda wakaenda kumpa pole. Kumbe Fisi na Sungura
walikuwa na lao jambo.
“Simba kwa kuwa huwezi kuwinda naomba unile mimi”, alianza kusema Sungura.
” Asante sana kwa kunijali, siwezi kukula wewe rafiki yangu. Sasa nimefahamu wewe ni rafiki yangu wa kweli katika kipindi hiki kigumu cha dhiki!” alijibu Simba.
Fisi naye akajitoa aliwe na Simba, ambaye pia alikataa kumla, akitoa sababu zilezile.
Sasa Punda akawa njia panda: “Nikikaa kimya nitaonekana mbaya kwa Simba. Kwanza Simba mwenyewe kakataa kuwala wenzangu, na mimi atakataa… acha
nijisemee tu kwamba najitolea anile…” aliwaza.
Akaropoka, “Simba kwa kuwa huwezi kuwinda naomba unile mi…” Kabla hajamaliza maneno yake alirukiwa na kuraruliwa palepale.
Kenya, Uganda , Rwanda na Burundi zina ajenda kadhaa kwenye EAF: mbali na zile “rasmi” zinazotangazwa hadharani. Ili ajenda zao zitimie, lazima “Punda” Tanzania awemo kwenye EAF ili aweze “kuliwa”.
Mheshimiwa Rais, ni wajibu na heshima kwako kuhakikisha Tanzania haijiungi na EAF kwa kuwa Tanzania haina ajenda mbali na ngonjera za kisiasa, pengine na posho za vikao kwa baadhi ya watu. Kwanza Tanzania siyo lazima ijiunge au ikubaliane na
kila kitu kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wachache wanaounga mkono kujiunga na shirikisho la afrika mashariki, wanadai upo umuhimu wa kujiunga kwa vile “dunia nzima mwelekeo ni kujiunga pamoja, kama
vile Jumuia ya Ulaya, EU”. Kama sababu ni hiyo, kwa nini tusibakie SADC tuliko? Hivi tulipigania uhuru wa kusini mwa Afrika ili iweje? Watanzania tulitoa damu zetu, mali na uhai wetu, kukomboa Ndugu zetu walio Kusini mwa Afrika, sasa ukombozi umepatikana, pana wakati gani muafaka zaidi ya huu kuendeleza undugu
wetu? Majirani zetu wa Afrika Mashariki tutaendelea kushiriana nao, kama tunavyoendelea kushirikiana na majirani zetu wengine. Kutojiunga kwenye shirikisho
siyo maana yake tutakuwa maadui!
Tanzania lazima ikae mbali na EAF, hata ikibidi kwa miongo kadhaa ijayo, ikiwa si moja kwa moja. Kwanza , Muungano wetu wenyewe una “mipasuko” ambayo haijasilibwa bado. Kabla ya kuulizwa kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, tuulizwe basi kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar . Tanganyika na Zanzibar , mara
baada ya kupata Uhuru, hazikutimiza miaka mitano, “zikaishia” na kuwa Taifa moja Tanzania . Sasa jamani, Tanzania hata miaka hamsini haijafikia, nayo “iishie”, tena kusikoeleweka? Tanzania ina manufaa tele SADC, kuliko kwenye shirikisho la Afrika Mashariki.

Hivi, wakati tulipokuwa “Mstari wa Mbele wa Ukombozi Kusini mwa Afrika”, majirani zetu wa Kenya na Uganda walikuwa wapi? Leo hii tukiwakubalia kuondoka SADC,
watatuona timamu kweli?
Mheshimiwa Rais Kikwete, kiasi inaeleweka ikiwa unaona pana ugumu wa wewe kuonekana unakwenda tofauti na Watawala wetu waliotutangulia, ambao huenda
wanapendelea kuona EAF ikizinduliwa, Tanzania ikiwemo.
Lakini mheshimiwa Rais, ndiyo maana kukawa na kikomo cha utawala cha vipindi viwiliviwili! Kwa kuwa umechaguliwa kwa ushindi “wa kishindo”, imani yetu
Watanzania imekuwa kwako kwamba utaweza kuipeleka Tanzania kule tunakotaka. Na tunakotaka sisi Watanzania siyo kwenye “soko la pamoja la afrika mashariki” wala EAF. Huo Muungano tu wa Forodha wa Afrika Mashariki unatekelezwaje? Matatizo na mizengwe iliyoko panaashiria nini pindi tukiwagaia nchi hii yote kwenye Shirikisho au “soko la pamoja”?

Siyo maafa, Mheshimiwa Rais?
Mheshimiwa Rais Kikwete, kwenye Jumuia ya Ulaya –EU, Uingereza na Jamhuri ya Ireland SIYO mataifa yaliyoko kwenye “Mkataba wa Schengen” wa Jumuia ya Ulaya,
mkataba unaoondoa mipaka na vizuizi baina ya nchi za Jumuia ya Ulaya kwenye masuala ya Uhamiaji, japo Uingereza na Jamhuri ya Ireland ni wanachama kamili wa
Jumuia ya Ulaya. Hii haikuzuia Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Ujerumani na nchi nyinginezo za EU zilizokubali kusaini kuendelea na “Makubaliano ya
Schengen”. Kadhalika , Iceland , Norway na Uswisi zimesaini “Mkataba wa Schengen” japo nchi hizo SI zanachama Jumuia ya Ulaya. Kila taifa linaangalia maslahi yake kama taifa.

Ulipoanzishwa umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki takriban karne moja
iliyopita, Tanganyika haikujiunga mpaka ilipoona vema kwamba itakuwa ni kwa maslahi yake kujiunga. Hii haikuzizuia Kenya na Uganda kuanzisha Umoja wao wa
Forodha. Tanganyika ilijiunga baadaye! Hata ile Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika, ilianzishwa baada ya kupita MIAKA HAMSINI tangu kuanzishwa ule
Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, japo nchi hizi zote tatu zilikuwa zinatawaliwa na Mkoloni mmoja takriban muda wote huo. Haraka ya sasa hivi ya nini?
Wanajua wakituachia muda, tukienda hatua kwa hatua, hawataweza tena kuigeuza Tanzania koloni lao. Tanzania iendelee kuwa mwanachama wa SADC, na kuendelea kuwa imesaini kwa muda makubaliano ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki mpaka pale SADC itakapoanzisha Umoja wa Forodha wa SADC, ambapo Tanzania itajitoa kwenye Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki. Au busara zaidi, ni vyema Tanzania ikajitoa SASA HIVI toka Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, na kuelekeza nguvu zake kwenye SADC. Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi zinaweza kuendelea na Umoja wao wa Forodha, Soko la Pamoja na Shirikisho (waliite vyovyote wapendavyo), bila Tanzania kuwemo.
Mheshimiwa Rais, ukubwa wa eneo la ardhi ya Tanzania ni zaidi ya Jumla ya eneo lote la ardhi ya Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi ukizichanganya pamoja — bila kuzungumzia rasilmali zilizoko. Halafu wanasema tuchanganye ardhi yetu na zao, halafu tugawane sawasawa kwa jina la “Soko la Pamoja la Afrika Mashariki”. Hivi tukikubali ujuha huo, ni kwa nini wasituone sisi mazuzu?
Swali kuu tunaloulizwa Watanzania na Tume yako mheshimiwa Rais ni iwapo Watanzania tunaona bado kuna sababu za Tanzania kuendelea kuwa nchi huru ambayo ni “dola”, wakati ambapo kuna shinikizo nchi yetu igawe uhuru wake kwa kisingizio cha “soko la pamoja” na “shirikisho la Afrika Mashariki”. Tuchukulie kwa
mfano, tume itawahoji na kupokea maoni toka kwa watu laki mbili. Kati yao 80% wakasema Tanzania ijiunge kwenye “Soko la Pamoja” na “Shirikisho la Afrika
Mashariki”, 20% wakasema tusijiunge. Je, Mheshimiwa Rais, hiyo itakuwa na maana uamuzi utakuwa umesilibwa wa Tanzania kufikia mwisho wake, kwa kujiunga na Soko
la Pamoja na Shirikisho la Afrika Mashariki?

Je, hutatumia busara kama ilivyotumika kwenye Tume ya Nyalali ya Vyama Vingi pale Tanzania ilipoangalia maslahi ya taifa, na kuruhusu mfumo wa vyama vingi, bila kuangalia asilimia zilizotokana na tume? Ikiwa kweli kabisa umedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye mwisho wake machinjioni Afrika Mashariki, kwa nini usiweke KURA YA MAONI kwa kila Mtanzania kupiga kura yake, badala ya kutumia Tume, angalau basi kuchelewesha kwa muda mauti ya Taifa Tanzania? “Soko la Pamoja” na pacha wake “Shirikisho la Afrika Mashariki” maana yake ni mwisho wa uhai wa Taifa la Tanzania . Ikiwa Tanzania itajinyonga (Mungu apishie mbali!) kwa kusaini mkataba wa “Soko la Pamoja la Afrika Mashariki” au ule wa “Shirikisho la Afrika Mashariki”, basi Watanzania tutasahau “maisha bora kwa kila Mtanzania” na itabidi tujiandae kwa “Bora Maisha kwa kila Mtanzania”, na kwamba wewe Rais wetu, Jakaya Kikwete, utakuwa umefeli vibaya kabisa jukumu lako la msingi tulilokupa — kulinda uhuru na umoja wa Taifa la Tanzania na kubakisha Taifa la Tanzania kuwa dola huru kwa manufaa ya Watanzania mpaka pale utakapomkabidhi madaraka ya Urais wa dola la Tanzania huru Mtanzania mwingine.
Kwa kuandika barua hii, imani yetu Watanzania kwako Rais wetu kwamba utaweza kuhimili mashinikizo yote ya nje, na kutusikiliza sisi raia zako, tunaotaka tubakie na taifa letu huru la dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Mwenyezi Mungu akujalie.

Amin.
Ndimi,
Mlenge Fanuel
Raia na Mwananchi wa Tanzania,
Simu: +255 75 4372902,
Email: mlenge@yahoo. com,
Dar es Salaam, Tanzania .

Advertisements

Entry filed under: Africa, Culture, Economics, Kenya, Literature, Media, Politics, Science, Society, World.

KBW : A year on In response: “Why I support Wiccanism”

2 Comments Add your own

 • 1. how to last longer for men  |  March 27, 2013 at 1:07 pm

  Hi I am so thrilled I found your site, I really found you by error, while I was
  browsing on Yahoo for something else, Regardless I am here now and would just like
  to say many thanks for a marvelous post and a all round interesting blog (I also love
  the theme/design), I don’t have time to
  read through it all at the moment but I have bookmarked
  it and also included your RSS feeds, so when I have time I
  will be back to read much more, Please do keep up the awesome
  work.

  Reply
 • 2. etsy.com  |  March 28, 2013 at 4:06 pm

  I was curious if you ever thought of changing the
  page layout of your blog? Its very well written; I
  love what youve got to say. But maybe you could a little more in the way of content so people could connect with it better.

  Youve got an awful lot of text for only having 1 or 2 images.

  Maybe you could space it out better?

  Reply

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Kenyan Analyst

Recent Posts

November 2006
S M T W T F S
« Oct   Dec »
 1234
567891011
12131415161718
19202122232425
2627282930  

Feeds


%d bloggers like this: